Bohari ya Dawa (MSD) imekabidhi vifaa tiba vya kisasa vya upasuaji kwa Kituo cha Afya cha Magazini kilichopo Kata ya Magazini Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 100.
Vifaa hivyo vinalenga kuwezesha kituo hicho kuimarisha huduma za afya kwa watu wenye magonjwa mbalimbali hasa yanayohitaji upasuaji.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa tiba hivyo, Meneja wa MSD Kanda ya Iringa, Robart Rugembe, amesema kuwa vifaa hivyo vitasaidia watu wengi ambao kwa sasa baadhi yao walikuwa wakisumbuliwa na magonjwa yanayohitaji upasuaji ikiwemo akina mama wajawazito.
Amevitaja baadhi ya vifaa vilivyopelekwa kwenye kituo hicho kuwa ni kitanda maalum cha kufanyia upasuaji, taa ambayo inatoa mwanga wakati wa upasuaji, vifaa vya uchunguzi, mashine ya kutakasa vifaa, vifaa vya kufulia nguzo na vifaa vya kukaushia vyombo, pamoja na mashine za upasuaji za kutosha.
Awali akipokea msaada huo, Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha Magazini, Dkt.Rashid Athuman amesema kituo hicho tangu kianze kufanya kazi hakijawahi kutoa huduma za upasuaji.