Vicky Nsilo Swai azikwa

0
167

Mazishi ya Vicky Nsilo Swai, aliyekuwa mke wa Mwanasiasa mkongwe, Mpigania Uhuru na Waziri wa zamani wa Tanzania Asanterabi Nsilo Swai, aliyefariki dunia Mei 31 mwaka huu yamefanyika katika kijiji cha Nkuusinde wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza wakati wa mazishi hayo, Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga amesema chama hicho kitaendelea kumuenzi Vicky Nsilo Swai, kwani alikuwa Mwanachama na Kiongozi muadilifu

Enzi za uhai wake, Vicky Nsilo Swai aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani Kilimanjaro kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2002 hadi mwaka 2012.

Pia aliwahi kuhifadhi nyumbani kwake viatu vya Mpigania Uhuru na Rais wa kwanza wa Afrika Kusini mwenye asili ya Afrika, Hayati Mzee Nelson Mandela, ambavyo aliviacha nyumbani kwa Mzee Nsilo Swai alipoingia Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 1962 akitokea Afrika Kusini ili kuanza harakati za ukombozi.