Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Geita, Japherson Nnko amesema, wanatarajia kuuboresha zaidi uwanja wa ndege wa Chato uliopo mkoani humo kwa kuuwekea uzio na kisha taa za kuongozea ndege.
Akizungumza na TBC mkoani Geita Nnko amesema, kibali cha kuuwekea taa za kuongozea ndege uwanja huo kimetolewa, lakini masharti ya Shirika la Kimataifa la Viwanja vya Ndege yanataka kabla ya kufunga taa kuwekwe uzio kuzunguka uwanja mzima.
Amesema maboresho kadhaa yanafanyika katika uwanja huo wa ndege wa Chato ili kukidhi vgezo vya kimataifa ikiwa ni pamoja na kujenga eneo maalum la kuegesha gari la zimamoto.
Meneja huyo wa TANROADS mkoa wa Geita ameongeza kuwa wataendelea na uboreshaji wa kiwanja hicho ili kuruhusu ndege zaidi kutua na kutoa huduma za usafiri wa anga kutokea katika uwanja huo.