Umoja wa Waganga wa Tiba Asilia, Tiba Mbadala na Wakunga wa Jadi nchini (UWAMATA) umesema kikundi cha watu wanaojiita Kamchape kwa madai ya kuwachapa wachawi mkoani Kigoma ni cha Matapeli waliyojivika kofia ya uganga.
Akizungumza katika uzinduzi wa ofisi ya chama hicho mkoani Kigoma,
Mwenyekiti wa
UWAMATA Taifa Mohamed Fundikila amesema, vitendo vinavyofanywa na watu hao havipaswi kufumbiwa macho, kwani ni udanganyifu na uchonganishi ambao unaweza kusababusha uvunjifu wa amani kwa jamii.
Aidha, Fundikila ameliomba Jeshi la Polisi kuendelea kuwasaka watu hao na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, huku akiwasisitiza Wananchi kutokubali kudanganyika.
Kwa upande wake Katibu wa Umoja huo mkoa wa Kigoma, Haruna Shaban na baadhi ya Waganga wamesema wanashangazwa na vitendo hivyo kwani hata namna vinavyofanyika ni tofauti kabisa na taratibu za matibabu ya tiba za asili.
Kauli ya UWAMATA
inakuja zikiwa zimepita siku chache baada ya kuibuka kwa kikundi cha watu ambao wanajiita kamchape na wengine Lambalamba ambao wanapita katika maeneo ya vijijini mkoani Kigoma wakichapa watu kwa tuhuma za ushirikina.