UVIKO19: Waliochanjwa kufanya kazi kwa uhuru

0
367

Mlezi wa wake wa viongozi wastaafu, Merry Majaliwa amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kupatiwa chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) ili waweze kufanya kazi zao kwa uhuru.

Merry ambaye ni mke wa Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa rai hiyo wakati akifungua zoezi la utoaji chanjo kwa wake za viongozi, wakuu wa vyombo vya habari na waandishi wa habari lililofanyika jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kupambana na ugonjwa huo.

Ameongeza licha ya kuwa chanjo ni hiari, lakini ni vyema wakafuata maelekezo ya wataalamu kwani wamethibitisha kuwa chanjo ni salama kwa binadamu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema kuwa chanjo ya UVIKO-19 italifungua Taifa kwa kuruhusu watu kuendelea na shughuli zao kama kawaida bila kuwa na hofu ya kuathiriwa na ugonjwa huo.

Akieleza umuhimu wa chanjo Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communication Limited, Bakari Machumu amesema chanjo ni sawa na mkanda kwenye gari kwamba ukifunga mkanda haimaanishi kuwa hautapata ajali, lakini utakusaidia kuepuka athari kubwa za ajali.

Vivyo hivyo chanjo haizuii mtu asipate maambukizi, lakini inamsaidia mtu kutoathiriwa sana kwani tayari mwili unakiwa umetengeneza kinga.

Kwa upande wake Mtangazaji wa TBC, Elizabeth Mramba akizungumza kwa niaba ya waandishi wa habari amesema waandishi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupokea chanjo hiyo ili wawe mabalozi wazuri kwa wananchi.

Amefafanua kuwa, mwandishi ambaye hajapata chanjo atakuwa hana uhalali wa kuhimiza wananchi kupata chanjo kwani watajiuliza kwanini yeye anayehamasisha hajachanjwa.

Katika zoezi hilo lililofanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam zaidi ya waandishi wa habari 200 wamechanjwa ikiwa ni pamoja na wake za viongozi.

Tanzania ilipokea dozi milioni 1 za chanjo ya Johnson & Johnson kutoka Marekani kupitia mpango wa COVAX ambao utaiwezesha Tanzania kupokea chanjo mbalimbali za kutosha asilimia 20 ya raia wote kutoka mataifa tajiri duniani.