Uteuzi wa Joyce Fisoo watenguliwa

0
436

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, – Susan Mlawi ameagizwa ampangie kazi nyingine Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza Nchini, – Joyce Fisoo na ateue mtu mwingine kushika nafasi hiyo.

Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akihitimisha kikao chake na zaidi ya wasanii Mia Moja kutoka Shirikisho la Filamu Tanzania.

Shirikisho la Filamu Tanzania linajumuisha vyama 11, ambapo 10 vimesajiliwa na kimoja hakijakamilisha usajili.

Vyama hivyo ni vya waigizaji, waongozaji, watayarishaji, wahariri, wachekeshaji, wapigapicha, waandishi wa miswada, watafutaji mandhari, wasambazaji wa filamu, walimu na chama cha wanawake wa tasnia ya filamu ambacho bado kiko kwenye mchakato wa usajili.

Kikao hicho kilichochukua muda wa zaidi ya saa saba, kilihudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bodi ya Filamu Tanzania pamoja na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wakiongozwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, – Juliana Shonza.

“Katibu Mkuu mtafutie eneo jingine la kufanya kazi, hana tuhuma zaidi ya mahusiano mabaya na wadau wake, ana historia nzuri, lakini tatizo ni mahusiano, mpeleke idara nyingine na hapa mlete mtu mwingine,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Filamu Tanzania, -Profesa Frowin Nyoni, Waziri Mkuu Majaliwa amemuagiza ajipange upya na Bodi yake na kuhakikisha kuwa wanatoa elimu kwa wasanii kama ambavyo imeainishwa kwenye sheria ya kuanzishwa kwa Bodi hiyo.

 “Bodi yako inao wajibu wa kutoa elimu kwa makundi tofauti ya wasanii, sheria yenu imeainisha kuwa mnapaswa kutoa elimu, wapeni mafunzo ili waongeze ujuzi na wakienda huko wanatoa uzoefu walionao kwa wanachuo, nao pia wanakuwa wamejifunza,” amesema Waziri Mkuu.

Kuhusu kukithiri kwa tozo ambazo zimelalamikiwa na wasanii wakati wa kikao hicho, Waziri Mkuu amesema kuwa kuna haja ya kulinda soko la ndani la kazi za wasanii wa Kitanzania tofauti na hali ilivyo sasa ambapo wazawa wanatumia gharama kubwa kutengeneza kazi zao lakini wanapata shida kuziuza ilhali wageni wanapata faida zaidi kwa kazi kama hizo.

 Kuhusu maudhui ya filamu zinazotengenezwa na wasanii wa Tanzania, Waziri Mkuu amesema kuwa inashangaza kuona masuala ya mapenzi yanaongoza kwenye filamu za Kitanzania kwa kushika nafasi ya kwanza ikiwa ni sawa na asilimia 68, vikifuatiwa na vichekesho ambavyo vinashika nafasi ya pili ikiwa sawa na asilimia 12.

Wakitoa maoni yao ni kwa nini tasnia ya filamu imedidimia, wasanii hao ambao waliwakilisha wenzao kutoka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Morogoro, Geita, Katavi na Rukwa wamedai kuwa Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza Nchini imeua tasnia hiyo, kwa hiyo hawana imani na Bodi hiyo na hawako tayari kufanya nayo kazi.