Utendaji wa Rais Magufuli katika kurasa 626 za kitabu

0
264

Vizazi hupita, barabara na masuala mbalimbali katika jamii, na historia yake husahaulika endapo haitatunzwa na kurithishwa kwa vizazi vinavyokuja. Kwa kutambua hilo, Taasisi ya Utafiti ya Umoja wa Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki na Kusini (ESAURP) imeandika kitabu kinachoelezea utendaji wa Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, kitabu kitachomtambulisha kwa vizazi vijavyo.

Kitabu hicho kilichoandikwa na watafiti 30 kutoka vyuo mbalimbali nchini kimepewa jina The Game Changer: President Magufuli’s First Term in Office ambapo kimechanganua na kuandika juu ya mafanikio ya kazi zilizofanywa na Rais Magufuli.

Akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), mhariri mkuu wa kitabu hicho, Profesa Ted Maliyamkono amesema Tanzania imekuwa na marais watano, kila mmoja alitenda mambo mazuri na makubwa, lakini kati yao hakuna aliyefanya mambo makubwa kwa muda mfupi kama Rais Magufuli, na hiyo ni moja ya sababu iliyowafanya kuandika kitabu hicho.

Miongoni mwa mafanikio ambayo kitabu hicho kimeelezea ni pamoja na mafanikio ya Tanzania katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona, Tanzania kufanikiwa kuingia katika kundi la nchi zenye uchumi wa kati miaka mitano kabla ya muda uliokuwa umekusudiwa, ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali kama vile reli ya kisasa (SGR), barabara, viwanja vya ndege, mapambano dhidi ya rushwa.

Mafanikio mengine ni uboreshwaji wa huduma za jamii ikiwemo; sekta ya afya, elimu bure, upatikanaji wa maji na kuongezeka kwa mapato ya nchi. Kuboreshwa kwa mikataba ya madini ambayo imeiwezesha nchi kunufaika zaidi na rasilimali zake, serikali kuhamia Dodoma na kuanza kujengwa kwa mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere katika Mto Rufiji.

Kitabu hicho kimeangazia masuala ya ndani ya nchi, hakijagusa mafanikio na changamoto za mambo ya nje katika kipindi cha awamu ya tano.

Januari 14, 2021 akizundua kitabu hicho, Waziri Mkuu aliwapongeza wanazuoni hao kwa kuona kazi nzuri iliyofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya Dkt. Magufuli na kuamua kuyaweka kitabuni.

‘’Haya yanayofanywa na Rais Magufuli ni lazima yawekwe kwenye historia ili wajukuu zetu hapo baadaye waweze kujua Rais wa awamu ya tano alifanya mambo gani mazuri katika uongozi wake,’ alisema Majaliwa.