Serikali imeboresha uratatibu wa kuandikisha wananchi wanaohama kwa hiari katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuwaandikisha katika ngazi ya kijiji wanapoishi.
Utaratibu huo ni tofauti na ule wa awali, ambapo timu moja iliyokuwa imeundwa na serikali ilikuwa ikipita kwenye maeneo ya vijiji vyote ndani ya hifadhi.
Kauli hiyo imetolewa na serikali kupitia mkuu wa wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, Raymond Mangwala wakati wa hafla ya kuagwa kundi la nane lenye kaya 25, wananchi 132 na mifugo 259 linalohamia katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga.
“Mwitikio kwa wanaojiandikisha umeongezeka sana, serikali imeboresha utaratibu na kuanzia wiki ijayo tumepanua wigo kwa wananchi kupiga simu kwa mtendaji wa kijiji ambaye atamuandikisha sehemu alipo, hii ni tofauti na ilivyokuwa awali kwa timu moja kuzungukia maeneo mbalimbali ndani ya eneo.” amesema Mangwala
Ameongeza kuwa baada ya mwananchi kuandikishwa na mtendaji wa kijiji, taarifa zitaunganishwa ngazi ya kata, tarafa hadi wilayani na baada ya hapo timu maalum itapita kwa ajili ya kufanya uthaminishaji wa nyumba na mali za mwananchi anayehama kwa ajili ya taratibu nyingine za serikali.
Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Needpeace Wambuya amesema, serikali kupitia mamlaka hiyo inaendelea kuratibu zoezi hilo kwa umakini na itawahamisha wananchi hao kwa awamu ili kuhakikisha mtu anayehama anapata huduma za msingi anakohamia ikiwemo nyumba, mashamba ya kulima, malisho ya mifugo, majosho na huduma mbalimbali za kijamii.
Aidha amefafanua kuwa katika kuongeza ufanisi wa zoezi hilo na kupunguza gharama za kuhamisha wananchi hao, magari ya serikali ndio yanayotumika kwa sehemu kubwa katika kusafirisha wananchi na mali zao.
Hadi kufikia leo, zaidi ya kaya 183 zenye wananchi 926 na mifugo zaidi ya 5,300 zimekwishahamia kwenye kijiji cha Msomera.