Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limeidhinisha Bilioni 35.4 ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Katika hotuba yake Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa amesema kati ya fedha hizo Bilioni 8.2 ni Mishahara, Bilioni 11.3 ni matumizi mengineyo na Bilioni 15.8 ni ya miradi ya Maendeleo.
Waziri Mchengerwa amesema katika idara ya maendeleo ya michezo yaliyoanza kufanyika ni kuanza kushughulikia tatizo sugu la miundombinu ya michezo ambayo kwa muda mrefu imekuwa na changamoto kama kuanza hatua za ujenzi wa Viwanja vya mazoezi na mapumziko (Recreational and Leisure Centres) vitatu katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Geita ambapo hatua zote za usanifu zimekamilika na sasa ujenzi utaanza mara moja
“Uamuzi wa kimkakati wa kujenga viwanja changamani vya michezo na sanaa (Sports and Arts Arena) katika mikoa ya Dodoma na Dar es salaam, umefikia hatua muhimu ambapo usanifu wa michoro (Architectural Design) umekamilika na sasa Serikali imetenga fedha za kuanza ujenzi lakini pia inazungumza na wadau wa sekta binafsi ili kutekeleza kwa pamoja ambapo sasa Tanzania inakwenda kuwa na Arena ya kwanza nchini zitakazokuwa na uwezo wa kuchukua wastani wa watu 16,000 kwa wakati mmoja” -amesema Waziri Mchengerwa.
Waziri Mchengerwa amesema katika mwaka wa fedha 2022/2023 Tanzania imepanga kushirikiana na Asasi ya Viacom CBS Network Africa and Peer Lead BET International katika maandalizi ya Tuzo maarufu za Muziki Barani Afrika zinazojulikana kama MTV Africa Music Awards.
Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Asasi ya (Music in Africa Conference for Collaborations, Exchange, and Showcases (ACCES) yenye Makao Makuu yake nchini Afrika Kusini inaandaa Mkutano wa Wadau wa Muziki Afrika utakaofanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Novemba, 2022.