Wizara ya Afya imesema kuwa wavutaji wa tumbaku wako hatarini kuyumba kiuchumi na kupata magonjwa yasiyoambukizwa kama tahadhari hazitachukuliwa mapema.
Waziri Ummy Mwalimu amesema utafiti uliofanywa nchini unaonesha kuwa kwa wastani matumizi ya tumbaku kwa mtu mmoja kwa mwezi yanagharimu shilingi 28,840, fedha ambayo inatosha kupunguza kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi kwa mtu mmoja mmoja kwa mwezi kwa 58% na umaskini wa kupindukia (mahitaji ya chakula) kwa mtu mmoja mmoja kwa mwezi kwa 85%.
“Kwa kutumia taarifa za matokeo ya viashiria muhimu vya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi kwa Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18, fedha za kujikimu kwa ajili ya mahitaji ya msingi kwa mwezi kwa mtu mmoja ni shilingi 49,320 na mahitaji ya chakula kwa mwezi kwa mtu mmoja ni shilingi 33,748,” amesema waziri huyo.
Utafiti wa matumizi ya tumbaku kwa watu wazima wa mwaka 2018 nchini umeonesha kuwa mtu mmoja kati ya 10 (8.7%), wenye umri wa miaka 15 au zaidi wanatumia tumbaku ya aina yeyote na hivyo kuwa na watu milioni 2.6 kati ya watu zaidi ya milioni 55 ambao wanaume ni 14.6% na wanawake ni 3.2%.
Aidha, watu 4 kati ya 10 (40.3%) nchini wamewahi kuona onyo la matumizi ya tumbaku kupitia redio au runinga. Pia matokeo ya utafiti yameonesha kuwa, watu 9 kati ya 10 (92.3%) wenye umri wa miaka 15 au zaidi wanaamini uvutaji wa sigara husababisha magonjwa, wakati watu 8 kati ya 10 (84.4%) wanaamini kuvuta hewa ya mtu anaevuta sigara kunaweza kuwasababishia magonjwa hata kama wao hawavuti sigara.
Katika kipindi cha miezi 12 iliyopita watu 4 kati ya 10 (32.9 wameathiriwa na moshi wa tumbaku sehemu za kazi ikiongozwa na sehemu za baa na kumbi za starehe kwa 77% (watu milioni 3), maeneo ya huduma za biashara za vyakula 31.1% (watu milioni 3.5) na majumbani 13.8% (watu milioni 4.1).
Wizara imesema utafiti huo una umuhimu wa kipekee kwani matokeo yake yatasaidia katika kutathmini hatua zilizofikiwa katika kupambana na magonjwa makuu manne yasiyoambukiza ambayo ni saratani, magonjwa ya moyo, magonjwa ya mfumo wa hewa na kisukari.