Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Japan,- Shinzo Abe na kuishukuru Japan kwa ushirikiano inaoutoa kwa Tanzania.
Wakati wa mazungumzo hayo yaliyofanyika mjini Tokyo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Tanzania inauheshimu na kuuthamini uhusiano huo mzuri kati yake na Japan.
Mazungumzo yao yamehusu masuala mbalimbali yakiwemo ya Kidiplomasia pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanywa kwa ushirikiano kati ya Japan na Tanzania.
Waziri Mkuu Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwakaribisha Tanzania Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Japan hasa wenye viwanda wawekeze nchini ili washirikiane na Watanzania kukuza uchumi.
Amesema Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imedhamiria kukuza uchumi na kufikia wa kati ifikapo mwaka 2025 kupitia sekta ya viwanda.
“Japan imepiga hatua kubwa katika teknolojia, hivyo naamini kuwa wafanyabiashara na wenye viwanda kutoka Japan wakiwekeza Tanzania wataleta tekinolojia yao pia,”amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.
Awali, Waziri Mkuu alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA), -Shinichi Kitaoka.
Katika mazungumzo hayo kiongozi huyo wa JICA alisema kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Tanzania kwa kutia saini mikataba mbalimbali yenye lengo la kuinua maisha ya Watanzania na kujenga uchumi.
Waziri Mkuu Majaliwa ameishukuru JICA kwa ushirikiano inaoutoa kwa Tanzania hasa katika
kuendelea kuwapokea Wanafunzi wa Kitanzania na kuwasomesha nchini humo katika taaluma mbalimbali.