Ushahidi kesi ya kina Mbowe waendelea kutolewa

0
289

Sajenti Goodluck Swai ametoa ushahidi wake unaoeleza mazingira ya ukamataji ya watuhumiwa Mohamed Ling’wenywa na Adam Kasekwa hadi walipofikishwa katika kituo kikuu cha polisi kati Dar es Salaam, 2020 kwa tuhuma za kula njama ya kutenda vitendo vya kigaidi.

Swai ni Shahidi wa tatu katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi namba 16 ya Mwaka 2021 ambayo ni uhujumu uchumi yenye mashtka ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake.

Akitoa ushahidi wake mahakamani hapo alipokuwa akihojiwa na Wakili wa Serikali, Pius Hila shahidi huyo ambaye ni Askari polisi idara ya upelelezi wa makosa ya jinai mkoani Arusha amedai alishiriki kuwakamata Ling’wenywa na Kasekwa eneo la Rau Madukani baada ya kupokea maelekezo kwa Afande Kingai.

Aidha, ameeleza mahakama hiyo kuwa baada ya watuhumiwa hao kukamatwa akiwa na Askari wenzake walipita maeneo ya Hoteli ya Aishi, Pasua Boma na maeneo meningine ya Arusha kwa lengo la kumtafuta mtuhumiwa mwingine Moses Lijenje bila mafanikio na mpaka sasa haijulikani alipo.

Amedai kwamba baada ya Lijenje kukosekana alishiriki kwenye zoezi la kuwasafirisha watuhumiwa kutoka Moshi hadi Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam na baadaye kituo cha Mbweni kwa maelekezo ya Afande Ramadhani Kingai.

Akihojiwa na Wakili wa Utetezi, John Malya shahidi huyo amedai baada ya gari la polisi kupata hitilafu ya umeme eneo la Himo, waliomba gari la RPC wa Kilimanjaro ili kuwasafirisha hadi kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam.

Kuhusu watuhumiwa kuteswa baada ya kukamatwa, shahidi huyo amedai sio kweli kwamba Ling’wenya na Kasekwa waliteswa katika vituo vya Moshi na Mbweni kama ilivyoelezwa hapo awali.

Afande Goodluck amedai baada ya kufika Kituo Kikuu cha polisi Dar es Salaam asubuhi ya saa moja alikabidhi vielelezo alivyochukua kutoka kwa Ling’wenya ambapo hata hivyo wote walikuwa katika hali nzuri bila malalamiko yoyote.

Baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake Mahakama imepokea kielelezo namba D1 ili kitumike kama kielelezo cha ushahidi kwenye kesi hiyo ndogo kwa upande wa utetezi.