Shahidi wa nne Anitha Mtaro mkazi wa Rau Madukani mkoani Kilimanjaro, katika kesi ya Uhujumu Uchumi na Ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe na wenzake watatu ameiomba mahakama kupokea fomu zenye taarifa za kushuhudia mshtakiwa wa pili Adam Kasekwa na Mohamed Ling’enywa
wakikamatwa eneo la Rau Madukani kwa tuhuma za ugaidi.
Akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Ester Martin kutoa ushahidi wake katika Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi iliyopo mkoani Dar es Salaam, shahidi huyo ametoa ombi hilo baada ya kufika mahakani hapo kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo kwa upande wa Jamhuri.
Shahidi huyo amedai kuwa Agosti 5 mwaka 2020 majira ya saa saba kasoro mchana akiwa eneo la Rau Madukani akitokea Saluni, aliwaona vijana watatu wakiwa na vijana wanaosajili laini za simu.
Baada ya muda kupita, shahidi huyo amedai aliwaona vijana wawili kati ya wale ambao alikuwa amewaona hapo awali wakiwa wanapita huku na kule wakiongea na simu, ghafla walitokea askari wawili ambao waliwaamrisha kuwa chini ya ulinzi kwa tuhuma za ugaidi.
Baada ya hapo walitokea askari wengine watatu eneo la tukio na kufanya idadi ya askari kuwa watano ambapo mmoja kati ya askari hao aliyejitambulisha kwa jina la Jumanne alifanya upekuzi kwa watuhumiwa na kukamata bastola yenye namba A 5340, risasi tatu na kete 58 za dawa za kulevya kwa mshtakiwa Adam Kasekwa.
Aidha shahidi huyo amedai kuwa mshtakiwa Mohamed Ling’wenywa ambaye ni mshtakiwa wa tatu katika shauri hilo alipekuliwa na askari na kukutwa na kete 25 zilizosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya, simu kubwa aina ya Tekno na laini za simu za kampuni ya Halotel na Airtel
Shahidi huyo ameeleza kuwa baada ya upekuzi huo kufanyika na watuhumiwa pamoja na mashahidi wa tukio kusaini fomu za mali zilizokamatwa kwa watuhumiwa hao, Adam Kasekwa na Mohamed Ling’enywa walivalishwa pingu kisha wakapelekwa kituo cha polisi Kati Moshi ambapo maelezo kwa watuhumiwa na mashahidi yalichukuliwa tena na kujazwa kwenye fomu.
Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala kwa pamoja wamesema hawana pingamizi na fomu hizo za maelezo na vielelezo vingine ikiwemo bastola, hivyo vipokelewe na mahakama kwa ajili ya utambuzi.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 2 mwaka huu kwa ajili ya mahakama kupokea ushahidi kwa shahidi wa tano kwa upande wa Jamhuri baada ya Mawakili wa pande zote mbili kupata wasaa wa kumuhoji shahidi wa nne.