Riaz Abedi kutoka Idara ya Elimu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) amesisitiza kwamba mfumo wa kupokea malalamiko shuleni ni kigenzo muhimu cha utekelezaji wa mradi wa Shule Salama za Sekondari nchini (SEQUIP).
Akitoa mafunzo kwa walimu wa sekondari kutoka mikoa ya Lindi, Morogoro na Dar es Salaam wanaohusika na utekelezaji wa SEQUIP yanayofanyika katika Manispaa ya Lindi, Riaz amesema ni vigumu kuwepo kwa utawala bora ikiwa hakuna nafasi ya kusikiliza na kupokea maoni, dukuduku na ushauri kutoka kwenye kundi linaloongozwa.
Umuhimu huo, amesema, unakuja kutokana na kigezo kwamba popote penye mtu zaidi ya mmoja kuna mawazo mbadala au tofauti juu ya jambo fulani hivyo ni vyema kuweka nafasi ya kupokea mawazo hayo ili kubaini na kutoa suluhisho pale ambapo kunajitokeza malalamiko au maoni.
Amesema Shirika la Fedha Duniani (IMF), mathalani, halipo tayari kutekeleza miradi ambayo ina viashiria vya kukandamiza watu, hivyo mfumo huo wa kupokea malalamiko unaouongozea sifa utekelezaji wa mradi wa SEQUIP kuendelea kupewa kipaumbele na shirika hilo.
Hata hivyo, amekumbusha kuwa sio tu IMF inayoamini katika kupata mrejesho wa wanaoongozwa bali hata Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ilishatoa waraka unaozitaka taasisi zote nchini zinazotoa huduma kwa wananchi kuwa na mfumo wa kupokea malalamiko katika maeneo ya kutolea huduma zao.
Amezitaja nyenzo na vifaa vya kupokea na kushughulikia malalamiko shuleni kuwa ni sanduku la maoni, dawati la ulinzi na usalama wa mtoto ndani na nje ya shule na kitabu maalumu cha kurekodi malalamiko.
Nyenzo nyingine amezitaja kuwa ni fomu maalumu ya kurekodi malalamiko, rejista ya malalamiko, uundaji na uendeshaji wa mabaraza ya watoto Tanzania pamoja na dawati la polisi linaloshughulikia ukatili wa jinsia na watoto