Waangalizi wa uchaguzi wa Rais na Wabunge nchini Ghana kutoka ndani na nje ya nchi hiyo wamesema kuwa, uchaguzi huo uliofanyika Disemba 7 mwaka huu ulikuwa huru na haki.
Waangalizi hao wametoa taarifa hiyo huku Kiongozi wa upinzani nchini Ghana, – John Mahama akipinga matokeo ya Urais yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo, kwa madai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na ukiukwaji wa taratibu.
Maafisa wa Chama cha upinzani cha National Democratic Congress wamesema kuwa wanafanya taratibu ili kuyapinga kisheria matokeo hayo.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, Rais Nana Akufo Addo aliyekuwa akiwania kiti hicho kwa kipindi cha pili ametangazwa mshindi baada ya kupata asilimia 51.59 ya kura zote zilizopigwa huku mpinzani wake wa karibu John Mahama ambaye ni Rais wa zamani wa nchi hiyo akipata asilimia 47.36 ya kura hizo.
Katika hotuba yake mara baada ya kutangazwa mshindi, Rais Nana Akufo-Addo ametaka kuimarishwa kwa mshikamano miongoni mwa raia wa Ghana na ameahidi kuinua hali za maisha ya Wananchi wa nchi hiyo.