Umeme wa gridi ya Taifa wazinduliwa Kigoma

0
902

Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali itahakikisha inaboresha upatikanaji wa huduma ya umeme mkoani kigoma, ili kuufanya mkoa huo kuwa na maendeleo na kuvutia uwekezaji.

Rais Samia ameyasema hayo mara baada ya kuzindua umeme wa Gridi ya Taifa wilayani Kasulu, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku nne mkoani Kigoma.

Rais Samia amezindua umeme huo wa Gridi ya Taifa na kuzima umeme wa jenereta uliokuwa ukitumika mkoani Kigoma kwa muda mrefu.

Pia Rais Samia amewataka wananchi wa mkoa wa Kigoma kulinda miundombinu ya umeme, ili iweze kuwapatia huduma ya umeme ya uhakika.

Akitoa taarifa kuhusu umeme huo wa Gridi ya Taifa uliozinduliwa hii leo, waziri wa Nishati January Makamba amesema umeme huo utakuwa mkombozi kwa wananchi wa Kigoma na utaokoa fedha nyingi za Serikali.

Awali Rais Samia Suluhu Hassan amezindua majengo mapya ya chuo cha ualimu cha Kabanga wilayani Kasulu, ambayo ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 14 na yamejengwa kwa msaada wa serikali ya Canada.