Ulega ashauri kuendelezwa mchezo wa bao

0
118

Mbunge wa jimbo la Mkuranga mkoani Pwani, Abdallah Ulega ameishauri jamii kuuendeleza mchezo wa bao, ili kumuenzi Muasisi wake, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Ulega ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ametoa ushauri huo wakati wa fainali ya mchezo wa bao aliouandaa ili kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika wilayani Mkuranga.

Amesema ni muhimu kuendeleza michezo ya jadi ukiwemo wa bao, kwa kuwa ni miongoni mwa michezo ambayo ni kielelezo cha Taifa.

“Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anahimiza michezo, na kuenzi historia ya jadi sana, Zanzibar hawajawahi kuacha jadi yao hata mwaka mmoja ambapo kila mwaka kuna maonyesho ya jadi na mwaka huu yeye mwenyewe alikuwa kinara kwenye michezo hiyo ya jadi maarufu kama Mwakakogwa ili kudumisha masuala ya jadi.” amesema Naibu Waziri Ulega

Kwa upande wake mgeni rasmi katika fainali hiyo ya mchezo wa bao ambaye ni mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Hadija Nasir amesema mchezo huo unaimarisha akili na kuleta furaha.

“Mwanzilishi wa mchezo huu hayati Mwalimu .Nyerere alidumisha mchezo huu na sisi tunapaswa kuuenzi.” amesema Nasir