Ulega aja na mkakato wa kuithaminisha zaidi dagaa

0
165

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema serikali imejipanga kuhakikisha inaboresha uvuvi wa dagaa hasusani katika Ziwa Victoria ili kuliongezea thamani zao hilo.

Ulega amesema hayo wakati wa mkutano na wadau wa Sekta ya Uvuvi wanaohusika na uchakataji wa minofu ya samaki na wavuvi kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita na Simiyu na kusisistiza kuwa serikali imejipanga kuupa thamani uvuvi wa dagaa ili kuongeza uwekezaji wa zao hilo.

“Tunataka tupate vichanja vya kutosha katika kuanika dagaa sio dagaa wanamwagwa tu inatakiwa wawekwe kwenye Vichanja,’’ amesema Ulega.

Amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaongea na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na wadau mbalimbali ili kuwekeza katika uvuvi wa dagaa.

Ameongeza kuwa dagaa wanatakiwa kupelekwa maeneo mbalimbali nchini na kusaidia kuondokana na tatizo la utapia mlo kwa kuwa dagaa wana madini mengi ya kutosha katika kuupatia mwili afya na kushauri viwanda mbalimbali kuhakikisha vinachakata dagaa vyema na kuuza ndani na nje ya nchi.

Naibu waziri Ulega amesema uvuvi wa dagaa umeleta ajira kwa watu wengi sana hususani akinamama hivyo ni muhimu kuhakikisha zao hilo linaendelea kuongeza tija zaidi katika kukuza pato la taifa na mtu mmoja mmoja.