Ulega aipongeza WWF

0
211

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (Mb) ameupongeza Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kwa kuyafanyia kazi maono ya serikali ya kuhifadhi mazao ya uvuvi ambayo yamekuwa yakiharibika kutokana na kukosekana kwa nyenzo za kuyahifadhi.

Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo akiwa katika Kijiji cha Songosongo kilichopo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi kituo cha kuzalisha barafu kilichojengwa na WWF kwa ufadhili wa Climateworks Foundation chenye thamani ya Shilingi Milioni 424, kwa ajili ya kuhifadhia samaki wanaovuliwa na wanakijiji hao.

Amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2021/22 imeweka mipango mbalimbali ya kuhakikisha inaongeza vituo vya kuhifadhia mazao ya uvuvi ili wavuvi waondokane na changamoto ya samaki kuharibika kutokana na ukosefu wa barafu na maeneo ya kuyahifadhia mazao hayo.

“Hali duni inachangiwa na upotevu wa mazao wanayovua kutokana na uvuvi na pia kutokuwa na uhakika wa masoko ya mazao wanayoyapata ndiyo maana serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inakuja na suluhu kuokoa wavuvi na watanzania kwa ujumla wake.” Amesema Ulega

Aidha, katika kuhakikisha mazao ya uvuvi yanakuwa na masoko ya uhakika Ulega amesema azma ya wizara hiyo ni kuona mazao hayo yanasimamiwa na ushirika hali ambayo itasaidia kuwa na umoja ambao utawezesha wavuvi kusikilizwa na kupata masoko kwa pamoja.