Ulega aagiza watendaji kusimamia maelekezo ya viongozi

0
199

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amesema atahakikisha kila maelekezo anayoyatoa anayafuatilia kwa karibu ili kujiridhisha na utekelezaji wake na kufikiwa kwa malengo ya serikali.

Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kujionea maendeleo ya ukarabati wa machinjio ya Jiji la Dodoma yaliyoanza tarehe 15 mwezi Julai mwaka huu.

Ulega amesema ameridhishwa na ukarabati unaoendelea kufanywa ambapo hadi sasa zimetumika Shilingi Milioni 40 kwa kutumia mapato ya ndani ya machinjio hayo.

“Kila maelekezo tunayoyatoa, tunayatoa kwa wakati maalum na kinachofuata ni ufuatiliaji wa karibu, tunatoa maelekezo na kufuatilia utekelezaji wake, tunawapongeza watendaji wetu wizarani maana kila maelekezo tunayoyatoa wanayasimamia na mnafanya kazi nzuri maelekezo tunayoyatoa mnayafanyia kazi.” Amesema Ulega

Ulega amesema alitoa maelekezo ya kuona machinjio ya jiji la Dodoma, yanabadilika na kuwa bora na kwamba ameridhika na ukarabati unaoendelea hadi sasa ambapo awali uongozi wa machinjio ulihitaji Shilingi Bilioni Tatu, lakini aliwaelekeza kuanza kufanya ukarabati kwa kutumia mapato ya ndani.

Amefafanua kuwa yeye kama kiongozi anatoa maelekezo na kuhakikisha yanasimamiwa usiku na mchana na kuyafuatilia hadi mwisho wake na kutaka maboresho hayo yawe yamekamilika kufikia tarehe 15 mwezi Septemba mwaka huu.