Mkurugenzi wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) anayesimamia majimbo ya Haut Katanga, Lualaba, Tanganyika na Lomami, René Masimango na ujumbe wake wametembelea Makao Makuu ya
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania
(TPA) pamoja na
bandari ya Dar es Salaam, ili kujionea shughuli mbalimbali za kiutendaji.
Wakiwa katika ziara yao, wameipongeza Menejimenti ya TPA na wafanyakazi wake kwa utendaji mzuri na kutoa huduma zenye ufanisi katika bandari zake.
“Bandari hii ya Dar es Salaam ni muhimu sana kwa mizigo inayokuja Congo na inahudumia mizigo mingi , tumekuja kuona utendaji kazi wake na tumeona kuwa kazi ni nzuri na bandari ina mipangilio mizuri.” Amesema Masimango.
Akiwakaribisha wageni hao, Mkurugenzi Mkuu wa TPA Plasduce Mbossa, amewashukuru kwa ziara yao na amewahakikishia kuwa Menejimenti yake ipo tayari kutatua changamoto zozote endapo zitajitokeza katika kuhudumia shehena ya mzigo unaoenda na kutoka Congo kupitia bandari za Tanzania.
Amesema lengo ni kulinda uhusiano mzuri na wa muda mrefu wa kidiplomasia na biashara kati ya nchi hizo mbili.
“ Menejimenti ya TPA itaendelea kuzifanyia kazi changamoto zozote Katika kuhudumia shehena ya Congo na kuboresha mahusiano ili shughuli zinazofanywa na TPA katika bandari zake ziwe na manufaa kwa DRC.” amesema Mbossa.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini DRC Said Mshana amesema, ziara hiyo ni fursa ya kuwa na majadiliano ya pamoja na yenye tija kuhusu changamoto zinazoyakabili mahusiano ya kibiashara na kutafuta suluhisho kwa manufaa ya Tanzania na DRC.
Naye Balozi wa DRC nchini Jean Pierre Massala amesema hiyo ni ziara muhimu kwa uhusiano kati ya DRC na Tanzania.
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ni kinara kwa kupitisha kiwango kikubwa cha shehena katika bandari za Tanzania hasa bandari ya Dar es Salaam.