Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa ujenzi wa vituo 350 vya afya utakuwa umekamilika nchi nzima ndani ya kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa serikali ya awamu ya Tano.
Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo mkoani Singida alipotembelea kituo cha afya cha Sokoine, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo yenye lengo la kukagua na kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Kulikuwa na hospitali 65 za wilaya, lakini tulivyoingia madarakani zimejengwa hospitali 67 na lengo kuu ni kuwapa wananchi huduma bora za afya”, amesema Makamu wa Rais.
Akiwa mkoani Singida, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan pia amezindua barabara ya Karume ambayo inajumuisha mradi wa mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita Sita Nukta Moja.