Mkuu wa Wilaya ya Muleba Toba Nguvila amesema ujio wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima Uganda hadi Chongoleani Tanga umeanza kuleta neema Wilaya humo kutokana na shughuli za maandalizi ya Ujenzi kuanza ikitajwa kuwa wataalamu mbalimbali waliofika maeneo ya Mradi kupata huduma mbali.
Akiongea kwenye mahojiano maalumu na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ofisini kwake Nguvila amesema, shughuli mbalimbali zimeanza na wakandarasi wa kampuni kadhaa zinazofanya Kazi kwenye Mradi huo wa EACOP wameripoti ofisini kwake na wanaendelea na shughuli za uandaaji wa Ujenzi wa Bomba hilo
Aidha Nguvila amesema kuwa Wananchi wa Muleba wameanza kunufaika na Mradi huo kutokana na nafasi mbalimbali za Ajira za kawaida huku akisisitiza Wananchi wengine kuendelea kujiandaa na fursa zitakazotokana na Mradi huo.
“Kuna waliolipwa pesa na wengine kutaka kujengewa nyumba, waliotaka pesa wamelipwa na Mkandarasi ameendelea kujenga nyumba tena ni nyumba bora na za kisasa kutoka nyumba duni kuanzia Kakoma hadi Muleba” ameongeza Nguvila
Nguvila ameongeza kuwa zaidi ya vijana 200 wamejitokeza kuomba kujiunga na jeshi la akiba la mgambo Ili kupata mafunzo ya ulinzi ili kulinda Mradi huo uliopita Katika Wilaya ya Muleba huku akisisitiza kuwa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ipo imara kulinda Mradi huo utakaokuza Pato la Taifa na Wananchi wa Muleba.
Serikali ya Uganga na Tanzania zimekubaliana kujenga Mradi huu wa kimkakati wa EACOP wenye urefu wa kilomita 1,445 ambapo kwa Tanzania pekee Bomba hilo litalazwa kwenye umbali wa kilomita 1,147 mpaka kufikia Chongoleani Mkoani Tanga ambapo mradi mzima unakadiriwa kutumia Dola za kimarekani bilioni 5.1 Sawa na zaidi ya shilingi za kitanzania trilioni 11.