Ujenzi shule ya msingi King’ongo waendelea kwa kasi

0
178

Siku moja baada ya Rais Dkt John Magufuli kuagiza kukarabatiwa kwa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi King’ongo iliyopo manispaa ya Ubungo jijini Dar es salaam, ukarabati huo umeanza kwa kasi.

Akizungumza katika mahojiano na TBC, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, – Beatrice Dominic amesema ujenzi pamoja na wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo hadi asubuhi hii umefikia asilimia tano huku mafundi wakiendelea na shughuli za kumwaga zege kwa ajili ya kuhakikisha ujenzi wa madarasa hayo unakamilika katika kipindi kifupi.

“Niombe radhi kwa hili lililotokea katika shule ya King’ongo iliyopo manispaa ya Ubungo, naomba niseme tumepokea maagizo yake [Rais] kwa haraka sana na tunaendelea kutekeleza na kama mnavyoona mafundi wako site,”amesema Beatrice.

Amesema ana orodha ya shule zenye changamoto ikiwemo miundombinu mibovu pamoja na uhaba wa madawati na tayari wameanza kuzifanyia kazi japo shule ya King’ongo haikuwepo kwenye orodha hiyo.

“Bahati shule hii ya king’ongo haikuwepo kwenye orodha kwa mujibu wa taarifa ya Afisa Elimu, lakini niseme hiyo sio excuse [sababu] ya kushindwa kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais,” amesema Mkurugenzi huyo wa Manispaa ya Ubungo.

Hapo jana Rais Dkt John Magufuli akiwa ziarani mkoani Kagera aligusia uchakavu wa majengo ya shule hiyo ya msingi King’ongo baada ya kusambaa kwa video ikionesha uchakavu huo na kutaka mamlaka zinazohusika kushughulikia jambo hilo na kuhakikisha Wanafunzi hawaki chini.