Ujenzi Ikulu ya Chamwino wafikia 91%

0
156

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameeleza kuridhishwa na ubora na maendeleo ya ujenzi wa Ikulu eneo la Chamwino mkoani Dodoma, na amemtaka mkandarasi ahakikishe mradi huo unakamilika Mei mwaka huu.

“Tunataka kumuwezesha Mheshimiwa Rais kufanya kazi katika eneo lake maalum na afanye kazi katika mazingira mazuri na kwa ufanisi.

Nimefurahishwa na taarifa kwamba ujenzi huu umefikia asilimia 91 na hatua iliyobaki hizi asilimia 9 ni kazi ndogondogo kama uwekaji wa milango, njia za mifumo ya hewa na umeme na zote zinaenda vizuri,” amesema Waziri Mkuu.

Amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kutekeleza ujenzi huo kwa ufanisi.

“Ramani iliyoko hapa iko sawasawa na jengo la Ikulu lililoko Dar es Salaam, wakandarasi wetu mmefanya kazi kubwa sana, hii imedhihirisha kuwa nchi yetu ina wataalam wa kutosha kujenga aina yoyote ya majengo.”

Kwa Upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania, Mhandisi Daudi Kondoro amemhakikishia Waziri Mkuu kwamba mradi huo utakamilika na kukabidhiwa mwezi Mei kama inavyotarajiwa kwani sasa uko katika hatua za mwisho za ukamilishaji.