Ujenzi daraja la Wami kukamilika Septemba 2022

Miundombinu

0
205

Ujenzi wa daraja jipya katika Mto Wami mkoani Pwani unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka 2022, ikiwa ni mwaka mmoja mbele kutoka muda wa awali wa kukamilika kwa mradi huo ambao ulikuwa ni Septemba 16, 2021.

Taarifa hiyo imeetolewa na Mhandisi Mshauri wa Mradi huo Gabriel Sangusangu kutoka kampuni ya Advanced Engineering Solutions Limited ya Tanzania wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa mradi huo kwa viongozi wa Mfuko wa Barabara Tanzania.

“Kwa ujumla maendeleo ya mradi yaliyofikiwa mpaka sasa ni asilimia 56.74, na muda wa mradi uliopita mpaka sasa ni takribani miezi 34, sawa na asilimia 97.64 ya muda wa mradi. Anguko kwenye ucheleeweshaji wa mradi mpaka sasa ni sawa na asilimia 40.9,” amesema Sangusangu.

Ametaja sababu zilizochangia mradi huo kutomalizika kwa muda uliopangwa kuwa ni pamoja na baadhi ya vifaa vya mkandarasi kuchelewa kufika eneo la kazi na uwepo wa mvua ambazo hazikutarajiwa.

Akiwa katika mradi Darajani hapo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Pwani, Mhandisi Andrea Kasamwa amesema wanaendelea kumsimamia mkandarasi kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa muda uliopangwa, ili kumaliza changamoto zinazotokana na matumizi ya daraja la zamani.

Daraja jipya la Wami ambalo ujenzi wake unagharimu shilingi bilioni 67.8, fedha ambazo zinatolewa na serikali, lina urefu wa mita 510 na upana wa mita 11.85 na linajengwa umbali wa mita 670 pembeni ya daraja laa zamani. Ujenzi wake unajumuisha ujenzi wa barabara za maingilio ya daraja kwa pande zote mbili zenye jumla ya urefu wa kilomita 3.8.