Uhuru wa habari ulindwe kwa sheria

0
187

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amefungua Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 linalofanyika mkoani Dar es Salaam na kusema kuwa wizara hiyo inaendelea na mchakato ili kuleta mabadiliko katika sheria na kanuni kandamizi.

Amewahakikishia waandishi wa habari nchini kuwa zitaundwa sheria bora zitakazosimamia na kulinda uhuru wa habari kwa miaka mingi ijayo.

“Uhuru wa habari nchini ni lazima ulindwe kwa sheria na sio utashi wa viongozi. Nia ni kuulinda uhuru huu kwa mujibu wa sheria hata kama hataki, alazimishwe na sheria.” amesema Waziri Nape

Ameongeza kuwa amani, maendeleo na furaha katika jamii huchangiwa pia na uwepo wa uhuru wa habari.

Aidha, Waziri Nape amewakumbusha waandishi wa habari nchini wajibu wao wa kuhabarisha lakini pia kulinda Taifa kwa ujumla.

“Tuna wajibu [wanahabari] wa kulinda nchi yetu, tuna wajibu wa kulinda rasilimali za nchi yetu.” amesema Waziri Nape

Ameeleza kuwa mwezi Januari mwaka 2023 marekebisho ya sheria ya huduma za habari yatawasilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.