Uhakiki wa mwisho wazinduliwa Namayakata

0
64

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limezindua zoezi la mwisho la uhakiki wa wananchi halali ambao maeneo yao yatachukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka eneo la uchimbaji la Ntorya kwenda kiwanda cha kuchakata gesi cha Madimba mkoani Mtwara.
 
Uzinduzi huo umefanywa na mkuu wa wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyobya  katika kijiji cha Namayakata wilaya ya Mtwara ambapo ujenzi huo unatarajia kuanza hivi karibuni.
 
Kyobya amewataka watendaji katika kata nne na vijiji 11 ambapo bomba hilo lenye utefu wa kilomita 35 litapita, kuhakikisha wanafanya uhakiki wa kina wa wananchi wanaostahili kulipwa fidia ili kuepuka migogoro ambayo inaweza kujitokeza wakati wa malipo au baada ya malipo.
 
Afisa Miliki Mwandamizi wa TPDC Happy Mwaseba amesema, uhakiki huo utalisaidia shirika hilo kuwalipa fidia watu sahihi ambao maeneo yao yatachukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo.
 
Amesema wananchi 253 katika vijiji 11 ambavyo bomba hilo litapita wameorodheshwa kwa ajili ya kulipwa fidia ya maeneo ya ujenzi wa bomba hilo kutoka Ntorya kwenda kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Madimba.