Ugonjwa usiofahamika waua watatu

0
180

Watu watatu wamefariki dunia mkoani Lindi, baada ya kuugua ugonjwa usiofahamika.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Alfello Sichalwe amewaambia waandishi wa habari mkoani Dodoma kuwa, watu hao watatu ni kati ya 13 waliougua ugonjwa huo.

Dkt. Sichalwe amesema ugonjwa huo umetokea katika halmashauri ya Ruangwa, ambapo kumeripotiwa ugonjwa usio wa kawaida kutoka Kituo cha afya Mbekenyera.

Amesema ndani kipindi cha siku 3 ambazo ni kuanzia tarehe 5 hadi 7 mwezi huu walipokea wagonjwa wawili katika kituo hicho wakiwa na dalili za homa, kuvuja damu hasa puani, kichwa kuuma na mwili kuchoka sana, na hadi kufikia tarehe 12 mwezi huu kulikuwa na wagonjwa 13, watatu ndio hao wamefariki dunia.

Profesa Sichalwe amesema
sampuli za awali zilizopimwa katika maabara ya Taifa zimeonesha majibu hasi kwa ugonjwa wa Ebola, Marburg na UVIKO-19.

Amesema uchunguzi zaidi wa kiepidemiolojia na kitabibu unaendelea, pia vinasubiriwa vipimo zaidi vya maabara ya magonjwa ya binadamu, wanyama na mkemia Mkuu wa Serikali.