Ufaransa yanunua bidhaa za dola Mil 25 Tanzania

0
92

Wawakilishi kutoka kampuni 27 za nchini Ufaransa wapo nchini kwa lengo la kukutana na wafanyabiashara wa Tanzania na kujadili namna ya kuboresha biashara na uwekezaji utakaonufaisha mataifa hayo.

Akizungumza mkoani Dar es Salaam wakati wa mkutano huo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe amesema mkutano huo ni mwendelezo wa mkutano uliofunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara nchini Ufaransa, ambapo alielekeza wafanyabiashara wa nchi hizo mbili washirikiane hasa katika maeneo ya kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo kupitia uchakataji wa viwandani.

Ameongeza kuwa biashara kati ya nchi hizo inaendelea kukua, huku Tanzania ikiagiza bidhaa kutoka Ufaransa zenye thamani ya takribani dola Milioni 75 za Kimarekani kwa mwaka na Ufaransa ikinunua bidhaa zenye thamani ya dola Milioni 25 kutoka Tanzania.

Naibu Waziri Kigahe amewaomba Watanzania kutumia fursa hiyo kuuza bidhaa zao na kufanya biashara zaidi na Ufaransa.

Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa nchini, Nabil Hajlaoui amesema uhusiano baina ya nchi hizo mbili umefikia kiwango cha juu kutokana na uthubutu wa viongozi wa mataifa hayo.

Amesema Tanzania ina fursa nyingi za vivutio vya uwekezaji, sera madhubuti na utulivu na kwamba kupitia mkutano huo watajenga uchumi mkubwa utakaonufaisha mataifa hayo mawili.

📸✍️ @kingdee255 (David Mayunga)

tbcdigital