UDOM, SUZA kukarabatiwa

0
178

Serikali ina mpango wa kujenga na kukarabati taasisi 23 za elimu ya juu nchini kikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kupitia mradi maalum wa elimu ya juu.

Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum Dkt. Thea Ntara aliyetaka kujua mpango wa serikali wa kukarabati chuo kikuu cha Dodoma na vyuo vingine ambavyo vilijengwa na kuonekana kuwa na dosari.

Naibu Waziri Kipanga amesema ukarabati huo utaenda pamoja na uboreshaji wa mtaala na kuanzisha mtaala mpya pamoja na kusomesha wahadhiri na kununua vifaa kwa vyuo vyote vikuu vya umma nchini.

Aidha Naibu Waziri Kipanga amesema kuna miradi mingine midogomidogo ambayo inaendelea kwa vyuo vya kati ili kuhakikisha vinakuwa na mazingira rafiki ya kufundisha na kujifunzia.

Hata hivyo Naibu Waziri Kipanga amesema kutokana na Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili kilichopo mkoani Dar es Salaam kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi, serikali itafungua kampasi mpya eneo la Mloganzila, Kigoma na Mbeya ambazo zote zitasimamiwa na Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili na mchakato wake umekwishakamilika.