UDART yatakiwa kuzingatia usalama barabarani

0
877

Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani Nchini Fortunatus Musilimu amewataka watendaji na wasimamizi wa mradi wa usafiri wa  mabasi yaendayo haraka jijini Dar es salaam (UDART)  kuzingatia sheria na taratibu zote za usalama barabarani.

Kamanda Musilimu ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam baada ya kukagua usalama barabarani kwa mabasi hayo yaendayo haraka katika eneo la Kimara.

Amesema kuwa mabasi hayo yanatakiwa kutopakia abiria wengi tofauti na uwezo wake, kuzingatia mwendo unaotakiwa katika kusafirisha abiria pamoja na kuzingatia alama za vivuko vya waenda kwa miguu zilizopo katika njia za mradi huo wa mabasi yaendayo haraka.

Naye mmoja wa viongozi wa UDART, –  Joe Beda amesema kuwa watazingatia maelekezo yote waliyopatiwa na Kamanda Musilimu, ili kuhakikisha usafiri wa  mabasi yaendayo haraka jijini Dar es salaam unakuwa salama na mfano wa kuigwa  katika kutekeleza sheria na alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazotokana na uzembe.

Nao baadhi ya wakazi walioshuhudia ukaguzi huo, wamekipongeza  Kikosi cha Usalama barabarani Nchini kwa kukumbusha kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani kwa wadau wote wa usafirishaji ili kuepuka na ajali zinazosababisha vifo na majeruhi.