Uchumi wa Tanzania haujashuka kwa miaka 10 iliyopita

0
295

Serikali imesema kuwa uchumi wa Tanzania haujawahi kushuka kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita ikiwa ni malengo ya nchi iliyojiwekea kwa muda wa kati na mrefu kwamba uchumi wake ukue kwa zaidi ya asilimia 6.

Takwimu hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amabaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi wakati alipofanya majadiliano juu ya masuala mbalimbali ya kitaifa.

Dkt. Abbasi amesema kuwa serikali imehamasisha watu kulipa kodi na inajitahidi kuhakikisha wananchi wanaiona thamani za kodi wanazozitoa. Amefafanua kuwa serikali hiyo ilivyoingia madarakani makusanyo ya kodi kwa wastani yalikuwa shilingi bilioni 850 kwa mwezi lakini sasa serikali inakusanya shilingi trilioni 1.5 kwa mwezi.

“Katika miaka mitano kazi kubwa imefanyika na sisi kama serikali tumetimiza wajibu wetu, tunaiona nchi yetu inaendelea kupata maendeleo kwa kasi. Uchumi wetu haujawahi kushuka kwa miaka 10 iliyopita, kwa takwimu za Benki ya Dunia (WB) kama hali ya ukuaji wa uchumi ikiendelea hivi huenda mwaka 2021 au 2022 tukaingia kwenye uchumi wa kati lakini ule wa chini kidogo”, alisema Dkt. Abbasi.

Aidha, ameongeza kuwa nchi haiwezi kupata maendeleo ya watu bila kuwekeza kwenye vitu, ndiyo maana awamu ya tano imewekeza kwenye vitu ikiamini vitachagiza maendeleo ya watu kwani kila sekta ambayo Serikali imewekeza inachangia katika kuleta mageuzi kwa wananchi wa kawaida kwa kutoa ajira. Kwa takwimu zilizothibitishwa sekta ya viwanda pekee imeajiri watu zaidi ya 200,000.

Akizungumzia kuhusu mradi wa bomba la mafuta, amesema kuwa mradi huo haujafa, ni wazo ambalo viongozi wamelipigania hivyo ni lazima litekelezeke. Kwa Tanzania hatua nyingi zimeshakamilika na kwenye mwezi Julai, 2020 Tenda zitaanza kutangazwa.