Uchumi wa Taifa waimarika licha ya janga la corona

0
216

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa, licha ya mlipuko wa ugonjwa wa corona ulioathiri uchumi wa nchi nyingi duniani, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizokuwa na ukuaji chanya wa uchumi kwa mwaka 2020.

Amesema pato la Taifa kwa mwaka huo lilikua kwa asilimia 4.8, ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.0 mwaka 2019.

Dkt. Mwigulu Nchemba ameyasema hayo Bungeni jiiini Dodoma wakati aliwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020, na mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2021/2022

Amesema ukuaji chanya wa uchumi ulitokana na
hatua ya Serikali ya kuruhusu shughuli za kiuchumi na kijamii kuendelea, na wakati
huohuo Wananchi wakisisitizwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Wataalam wa afya.

Aidha, amesema kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi nchini kulichangiwa na athari za corona katika nchi washirika wa kibiashara, pamoja na mafuriko yaliyosababisha uharibifu wa miundombinu ya usafirishaji na kuchelewesha
utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo.

Dkt. Nchemba amesema athari za janga la corona zilijitokeza zaidi katika
shughuli za kiuchumi za malazi, huduma ya chakula pamoja na sanaa na burudani ambazo zilikuwa na ukuaji hasi kwa mwaka 2020.