Uchaguzi wa Babati Mjini na Ukerewe nao kufanyika Disemba Pili

0
2424

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo kwenye majimbo mawili na kata 26 za Tanzania Bara.

Majimbo hayo ni Babati Mjini lililopo halmashauri ya mji wa Babati mkoani Manyara na jimbo la Ukerewe katika halmashauri ya wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza

Makamu Mwenyekiti wa NEC Jaji Mbarouk Salum Mbarouk amesema kuwa uchaguzi huo utafanyika pamoja na uchaguzi wa jimbo la Simanjiro mkoani mkoani Manyara na Serengeti mkoani Mara pamoja na kata 21 za Tanzania Bara uliotangazwa  awali.

“Nafasi hizo wazi zimetokana na waliokuwa Wabunge wa majimbo hayo Joseph Mkundi (Ukerewe) na Pauline Gekul (Babati Mjini) kujiuzulu kutoka kwenye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),” amesema Jaji Mbarouk.

Jaji Mbarouk amesema  kuwa fomu za uteuzi  wa  wagombea zitatolewa kati ya  tarehe 28 mwezi huu na  tarehe tatu Novemba mwaka huu, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe tatu Novemba mwaka huu, kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe nne Novemba  hadi Disemba Mosi na siku ya uchaguzi ni tarehe Pili Disemba mwaka huu.

Ametoa wito kwa wadua wa uchaguzi nchini kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi chote cha uchaguzi huo mdogo.