Uchaguzi mdogo wa Ubunge Liwale Oktoba 13

0
2381

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewasihi wapiga kura wote waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na wanaoishi kwenye jimbo la Liwale mkoani Lindi na kata nne za Tanzania Bara kujitokeza kupiga kura Jumamosi Oktoba 13 mwaka huu ili kuwachagua viongozi wanaowataka wawaongoze kwa kipindi cha takribani miaka miwili ijayo.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage  na kuwataka wapiga kura hao kutokua na hofu, woga ama wasiwasi wa aina yoyote.

Mbali na wito huo, Jaji Kaijage  pia amewataka wakazi wa jimbo hilo la Liwale na wa kata hizo nne, vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kushirikiana ili kuhakikisha kuwa viashiria vya kuvunjika kwa amani na utulivu vinaepukwa ili uchaguzi utakaofanyika uwe huru, wazi na wa haki.

“Wananchi waheshimu sheria za nchi wakati wote wa upigaji, kuhesabu, kujumlisha kura na kutangaza matokeo, pale panapokuwa na malalamiko yoyote ya ukiukwaji wa sheria na taratibu za uchaguzi, malalamiko hayo yafikishwe kwenye mamlaka inayohusika kwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria.”, ameongeza Jaji Kaijage.

Amesisitiza kuwa ni wajibu wa vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi huo  mdogo kuweka mawakala katika vituo vyote vya kupigia na kujumlishia kura kwa utaratibu ambao umekuwa ukitumika katika chaguzi za hivi karibuni.

Uchaguzi huo mdogo wa bbunge katika Jimbo la Liwale mkoani Lindi  na udiwani katika kata nne za Tanzania Bara unafanyika kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujiuzulu kwa mbunge na madiwani wa kata hizo na utahusisha zaidi ya wapiga kura elfu 69  walioandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura na kutakuwa na vituo vya kupigia kura 192.