Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inatarajia kufanya zoezi la uandikishaji Wapiga Kura kwa majaribio katika kata mbili za Kibuta iliyopo kwenye Halmashauri ya wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani na Kihonda katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa NEC Jaji Semistocles Kaijage imesema kuwa, uandikishaji huo wa majaribio utakaoanza Machi 29 hadi Aprili Nne mwaka huu, utafanyika katika vituo 20 vya kuandikisha Wapiga Kura ikiwa ni vituo 10 katika kila kata.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uandikishaji huo unalenga katika kuvifanyia majaribio vifaa na mfumo wa uandikishaji Wapiga Kura ili kubaini changamoto kabla ya kuanza rasmi kwa zoezi hilo.
Imezitaja sifa za watu watakaoandikishwa kuwa ni raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 au atakayetimiza umri wa miaka 18 siku ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Uandikishaji huo hautawahusu raia walio chini ya kiapo cha utii wa nchi nyingine, aliyebainika kuwa hana akili timamu au yuko kizuizini kama mhalifu mwenye ugonjwa wa akili au yuko kizuizini kwa ridhaa ya Rais.
Taarifa hiyo imeendelea kutaja watu ambao hawatahusika katika majaribio hayo ya uboreshaji kuwa ni aliyehukumiwa adhabu ya kifo na mahakama au anatumikia kifungo kinachozidi miezi sita pamoja na mtu aliyepoteza sifa za kuandikishwa kuwa Mpiga Kura chini ya Sheria za Uchaguzi au Sheria nyingine yoyote inayohusu makosa ya uchaguzi.
Wakati huohuo NEC imetoa fursa kwa Vyama vya Siasa nchini kuweka Wakala mmoja katika kila kituo cha Kuandikishia Wapiga Kura kwa lengo la kushuhudia na kujiridhisha juu ya taratibu zitakazotumika pamoja na changamoto zitakazojitokeza ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kabla ya kuanza kwa zoezi rasmi la Uandikishaji.