TUNAWEKEZA ZAIDI KWENYE SEKTA KIPAUMBELE

0
257

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Tanzania inalenga kuongeza uwekezaji katika sekta za kipaumbele ikiwemo elimu, afya na huduma nyingine za kijamii, ikiwa ni pamoja na kilimo cha kisasa kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi kama hatua ya kukuza uchumi endelevu na kupunguza umaskini.

Ameyasema hayo visiwani Zanzibar wakati akifungua mkutano wa kitaalamu wa Benki ya Dunia wa Mapitio ya Kati ya tathmini ya utekelezaji wa mzunguko wa 20 wa mfuko wa IDA unaofanyika visiwani humo kwa siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine utajikita kufanya tathmini ya miradi inayotekelezwa katika nchi zenye kipato cha chini kupitia fedha za mkopo na msaada zinazotolewa na mfuko huo uliopo chini ya Benki Dunia.

Akiangazia msaada wa IDA katika kusaidia mabadiliko ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania Rais Mwinyi amesema ufadhili umechangia kwa kiasi kikubwa katika kusaidia utekelezaji wa miradi Tanzania Bara na visiwani akiweka wazi baadhi ya miradi ikiwemo mradi wa nishati ya umeme vijijini wenye thamani ya dola milioni 200 ambao umewezesha Tanzania kufikia watu zaidi ya milioni 2.5 kupata nishati ya umeme na dola milioni 335 ambazo pia zimetumika katika uboreshaji na ujenzi wa vituo vya afya na madarasa .

Hata hivyo Rais mwinyi ameiomba Benki ya Dunia kupitia dirisha la IFC na IDA kuangalia namna ya kukopesha sekta binafsi ili kuwezesha ushindani wa biashara katika eneo huru la biashara Afrika hatua itakayochochea ongezeko la ajira kupitia ushirikiano wa kikanda na biashara.

Kwa upande wake Rais wa Benki ya Dunia, Ajay Banga anasema kabla ya 2030 IDA itatoa dola za Marekani bilioni 5 kama dhamira ya kufikisha umeme wa uhakika, nafuu, na mbadala kwa Waafrika milioni 100.

Kwa mujibu wa tovuti ya Benki ya Dunia katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2023, Tanzania ilikuwa miongoni mwa wakopaji 10 bora ambapo ilinufaika na mkopo wenye masharti nafuu wa dola bilioni 2.13.