TUNAPUNGUZA VIFO VYA WATOTO WACHANGA

0
211

Taasisi ya Doris Mollel Foundation imetoa vifaa tiba kwa ajili ya kuanzisha Wodi ya Watoto Wachanga Mahututi (Neonatal Intensive Care Unit) ikiwemo watoto njiti katika Hospitali ya Masiwani, Halmashauri ya Jiji la Tanga.

Akipokea vifaa hivyo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa mwelekeo wa Serikali ya awamu ya sita kwa upande wa afya ya uzazi, mama na mtoto ni kujikita katika utoaji wa huduma bora kwa watoto wachanga hususan watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) ili kupunguza vifo vya watoto wachanga.

Waziri Ummy ameipongeza na kuishukuru Taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha Tanzania inafikia Malengo Endelevu ya Milenia ya kupunguza vifo vya watoto wachanga hadi kufikia vifo 12 kwa kila vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2030 kutoka vifo 24 kwa kila vizazi hai 1,000 kwa sasa.