Tumuenzi Musuguri kwa kuwa tayari kuifia nchi

0
29

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amewataka Watanzania kumuenzi Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali David Musuguri, kwa kuonesha uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yao na kuwa tayari kujitoa, hata ikibidi kufa kwa ajili ya kulinda na kutetea uhuru, heshima na maslahi ya Taifa.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa kuaga mwili wa Jenerali Musuguri katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo Jijini Dar es salaam. Ametoa rai hasa kwa vijana wa Tanzania kuipenda nchi na jeshi la Tanzania kwa moyo wote na kuwa tayari kuilinda Tanzania kwa gharama yoyote ile kama alivyofanya Jenerali Musuguri.

Amesema makamanda na wapiganaji waliopewa dhamana ya uongozi katika jeshi hawana budi kuendelea kufuata mfano bora uliyoachwa na Jenerali Mstaafu, David Musuguri.

Dkt. Mpango mesema Musuguri alilipenda sana jeshi maisha yake yote na alikuwa mwalimu na mlezi makini wa askari vijana. Amesema alipopewa jukumu la kuongoza Jeshi la Wananchi wa Tanzania alifanya jitihada kubwa kulijenga na kuliendeleza jeshi na kulifanya kuwa kati ya majeshi bora na imara barani Afrika na ndiyo maana Jeshi la Idd Amin Dada aliyekuwa Rais wa Uganda lilipovamia kipande cha ardhi ya Tanzania lilidhibitiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) likiongozwa na Musuguri.

Makamu wa Rais ametoa salamu za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali nzima kwa Mkuu wa Majeshi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa ujumla, familia, ndugu wa Marehemu na Watanzania wote kwa msiba huu mkubwa kwa Taifa.

Amesema Serikali inaiombea faraja familia ya hayati Musuguri ambaye wakati wa Vita ya Kagera dhidi ya Uganda mwaka 1978-1979 alijulikana kama “General Mutukula” ambao ulikuwa mji muhimu kimkakati na wote walioguswa na msiba huu na kuwahakikishia kwamba Serikali na Taifa zima lipo pamoja nao.