Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Albert Msando amesema wanafunzi katika kijiji cha Msomera wana madarasa na madawati ya kutosha, na kwamba Serikali imewapatia shillingi Millioni 260 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya shule ya sekondari.
Msando amesema hayo alipokuwa akisoma taarifa ya Wilaya ya Handeni wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Batilda Burian, ziara iliyokuwa na lengo la kuwatembelea wananchi wa kijiji cha Msomera ambao wamehamia kwa hiari wakitokea eneo la Hifadhi ya Taifa Ngorongoro.
Amesema mabweni hayo yatawawezesha wanafunzi kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shule.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ya Handeni amesema Serikali imeahidi kujenga shule mpya ya msingi katika kitongoji cha Mkabalu.