Tume ya Madini yatembelea machimbo ya Mpwapwa

0
2200

Mwenyekiti wa Tume ya Madini nchini Profesa Idris Kikula ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Afisa Madini na Mwenyekiti wa Chama Cha Wachimbaji wadogo wa madini mkoa wa Dodoma kumaliza mgogoro kati ya wachimbaji wadogo na Mwekezaji kwenye machimbo ya Winza yaliyopo wilayani Mpwapwa, mgogoro uliodumu kwa takribani miaka Kumi.

Profesa Kikula ametoa muda huo baada ya kupata malalamiko ya
wachimbaji hao wadogo ya kushindwa kuendelea na shughuli za uchimbaji kutokana na mgogoro uliopo baina yao na mwekezaji katika eneo hilo, hali ambayo pia inaikosesha serikali mapato.

Wachimbaji hao wadogo wametoa malalamiko hayo kwenye Tume hiyo ya Madini nchini inayoongozwa na Profesa Kikula ambayo imefanya ziara katika machimbo mbalimbali wilayani Mpwapwa ili kujionea shughuli za uchimbaji wa madini na namna serikali inavyoweza kufaidika na shughuli hizo za uchimbaji.

Wakizungumza na wachimbaji hao, baadhi ya wajumbe wa Tume hiyo ya madini nchini wamewashauri wachimbaji hao wadogo kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria wakati malalamiko yao yakifanyiwa kazi

Wajumbe wa Tume hiyo ya madini nchini wanaendelea na ziara yao katika wilaya za Mpwapwa na Kongwa mkoani Dodoma.