TRA yatakiwa kuzingatia sheria katika kukadiria kodi

0
191

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwingulu Nchemba ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutumia weledi na kuzingatia sheria katika kukadiria kodi kwa Wafanyabiashara ili kulinda walipa kodi na kutanua wigo wa walipa kodi.

Dkt. Nchemba ametoa agizo hilo jijini Dodoma alipokutana na wakuu wa Idara na Taasisi za wizara hiyo, katika kikao kazi kilicholenga kutekeleza maelekezo yaliyotolewa hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan.

Miongoni mwa maagizo hayo ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuitaka wizara hiyo ya Fedha na Mipango kutatua changamoto za Wafanyabiashara nchini kuhusu masuala ya kodi.

“Maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni muhimu yatekelezwe ipasavyo ili kulinda na kukuza uchumi wa nchi kwa kutoza kodi kwa staha, weledi na kwa mujibu wa Sheria na turekebishe mahali tulipoharibu,”amesisitiza Dkt. Nchemba.

Ameitaka TRA kuacha kudai taarifa za miaka ya nyuma ambayo iko nje ya sheria kwa Wafanyabiashara ambazo zilikwishafanyiwa kazi, kwani utunzaji wa kumbukumbu ni changamoto kwa wengi.

“TRA nawataka mpeleke ujumbe makini kwa Wafanyakazi wa TRA nchini nzima, kwamba Serikali haijasema msikusanye kodi au mpunguze jitihada za kukusanya kodi hizo bali kinachoongelewa na kusisitizwa ni kukadiria na kukusanya kodi kwa kuzingatia sheria na taratibu, bila kuonea watu,”amesema Dkt. Nchemba.

Ameongeza kuwa ili kuendelea kupata mapato ya kutosha nchini, ni lazima kuwalea Wafanyabiashara ili kuwajengea uwezo wa kiuchumi akitolea mfano wa ng’ómbe wa maziwa anayetakiwa kupewa huduma muhimu kabla ya kumkamua maziwa.

“Mheshimiwa Rais alielezea changamoto ya kushika akaunti, fedha za Wafanyabashara, tuache vitendo hivyo, hapa hakuna mjadala ni lazima yafuatwe na sisi Wizara tutaendelea kufuatilia maelekezo hayo” amesema Dkt. Nchemba.

Amesisitiza TRA kuzingatia maelekezo aliyotoa na kurekebisha pale ambapo sheria hazikuzingatiwa, ili kulinda uchumi wa nchi na kutodhoofisha biashara za walipakodi pamoja na kuangalia namna ya kuongeza walipa kodi wapya.

Waziri huyo wa Fedha na Mipango pia ametoa rai kwa Watanzania wote kulipa kodi inayostahili kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo na kuzingatia matumizi bora ya kutunza kumbukumbu za malipo.