Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeendelea kuboresha miundombinu yake katika visima vya Songosongo mkoani Lindi, na hivyo kuwezesha kuzalisha zaidi nishati hiyo inayotegemewa kuzalisha umeme kwa zaidi ya asilimia sitini.
Akizungumza na Mwandishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mara baada ya kukagua maboresho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Dkt. James Mataragio amesema maboresho hayo yamelenga kukarabati visima vya zamani na kuweka mtambo mpya unaotumika kuongeza mgandamizo wakati wa uzalishaji wa gesi asilia.
Dkt. Mataragio amesema kuwa, maboresho hayo ya visima na kuongeza mtambo mpya yamesaidia kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi asilia kutoka futi za ujazo milioni 90 za awali kwa siku hadi kufikia futi za ujazo milioni 140 kwa siku.
“Maboresho ya visima vitatu yamefanyika ikiwa ni kisima namba 3, namba 4 na namba 10 ambavyo vilikuwa vinazalisha lakini uwezo wa kuzalisha ulipungua, na pia tunaendelea na uwekaji wa mtambo mpya wa kuongeza mgandamizo kiwandani hapa.” ameongeza Dkt. Mataragio
Kwa upande wake Meneja uzalishaji wa kiwanda cha kuzalisha gesi asilia cha Songas, Elias Mnunduma amesema mara baada ya maboresho ya visima na kufunga mtambo wa kuongea mgandamizo, TPDC na Pan Africa Energy (PAET) wataendelea kuzalisha gesi asilia zaidi na kuisambaza kwa watumiaji kulingana na mahitaji ya wateja wao.
Aidha Kaimu Meneja Mkuu wa GASCO Mhandisi Baltazar Mroso amesema kwa sasa asilimia mia moja ya wataalam wanaoendelea kusimamia mitambo ya uzalishaji wa gesi asilia ni wazawa ambao wamepata ujuzi wa kutosha katika kusimamia kazi zote za uzalishaji wa nishati hiyo tofauti na hapo awali ambapo sehemu kubwa walikuwa wakisimamia na kuendesha wataalam wa kigeni.