TPDC na mkoa wa Pwani wakubaliana kushirikiana zaidi

0
163

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na mkoa wa Pwani wamekubaliana kuzidisha ushirikiano katika kukuza uwekezaji wa viwanda na uzalishaji wa bidhaa hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio walipofanya kikao kazi katika ofisi za Sekretari ya Mkoa wa Pwani zilizoko Kibaha.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Mataragio amesema Mkoa wa Pwani unashika nafasi ya pili kwa idadi ya viwanda vinavyotumia gesi asilia hapa nchini na mahitaji yanaonekana kuendelea kukuwa kwa kasi.

“Utafiti wetu umebaini takribani viwanda 25 vyenye kuhitaji gesi asilia eneo la viwanda Zegeleni-Kibaha ambapo tunategemea kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni 17 kwa awamu tofauti kuwafikia wateja hawa kwa njia ya gesi iliyoshindiliwa (CNG),” amesema Mkurugenzi wa TPDC

Kwa upande wake RC Kunenge ameeleza mpango wa Mkoa wa Pwani kufanya mageuzi makubwa ya kutumia rasilimali zilizopo ndani ya mkoa huo kunyanyuka kiuchumi ambapo nishati ya gesi asilia ni sehemu ya mpango huo na hivyo kusisitiza ushirikiano zaidi baina ya ofisi yake na TPDC.

“Tunataka kufanya mageuzi makubwa ikiwemo kuhimiza wenye viwanda kuongeza uzalishaji kuendana na uwezo wa kiwanda ili kutoa ajira zaidi kwa watu wetu na pia kuongeza mapato ya Serikali, na katika hili tunajua nishati ni sehemu muhimu kutusaidia kufikia uzalishaji wa kiushindani,” ameeleza Kunenge