TPDC kuendelea kujidhatiti kwenye biashara ya mafuta

0
304

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dkt. James Mataragio amesema shirika hilo litaendelea kujidhatiti katika biashara ya mafuta hapa nchini kupitia kampuni yake ya TANOIL, ili kuhakikisha nchi haiingii katika uhaba wa mafuta.

Dkt. Mataragio ameyasema hayo mkoani Dar es salaam mara baada ya kufanya ziara ya kukagua hifadhi ya mafuta eneo la kigamboni, ambapo TANOIL ndio kampuni tanzu ya TPDC inayohifadhi bidhaa hiyo.

Amesema Serikali kupitia TPDC na kampuni tanzu ya TANOIL imerudi kwenye biashara ya mafuta, ikiwa ni takribani miaka 21 tangu ilipoacha kujihusisha na biashara hiyo moja kwa moja.

Kwa mujibu wa Dkt. Mataragio, kurudi kwa TPDC kwenye biashara ya mafuta hakuiondoi sekta binafsi, bali inakuja kushiriki kama kampuni binafsi zinavyoshiriki chini ya usimamizi wa sheria na kanuni zilizopo.

“Lengo letu ni kuhakikisha bidhaa hii ya mafuta inapatikana wakati wote kuepuka uhaba sokoni ambayo ni hatari kwa usalama wa nchi, na TPDC ina jukumu la kisheria kuhakikisha wakati wote nchi ina hifadhi ya mafuta ya dharura na hii ni sehemu ya utekelezaji wa takwa hilo la kisheria” amefafanua Dkt. Mataragio