TPA yatakiwa kusimamia ujenzi wa miundombinu ya bandari

0
163

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amezitaka taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kutatua kero na malalamiko ya Wananchi kwa wakati katika miradi na huduma wanazozitoa.

Akizungumza mkoani Rukwa mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga Port yenye urefu wa kilometa 112 na upanuzi wa bandari ya Kasanga, Naibu Waziri Kasekenya ameridhishwa na kazi inayofanyika na kumtaka Mkandarasi China Railway 15 Group kukamilisha sehemu iliyobaki yenye urefu wa mita 150 katika kipindi cha siku 45.

Aidha, amemtaka Mkandarasi Shanxi Construction Engineering anayetekeleza mradi wa upanuzi wa bandari ya Kasanga kutathmini kazi anayoifanya kama iko katika viwango vinavyokubalika kwa mujibu wa mkataba kabla ya kuchukuliwa hatua.

“Hakikisheni kazi za ujenzi wa barabara na upanuzi wa bandari zinakamilika katika kipindi kifupi kuanzia sasa, kwa kuwa muda uliopangwa kimkataba umemalizika”, ameagiza Naibu Waziri Kasekenya.

Naibu Waziri huyo amemuagiza Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Meneja wa Bandari ya Kigoma kufika eneo la mradi ndani ya kipindi cha wiki moja kwa ajili ya kukagua maendeleo ya mradi huo na kutoa ripoti.

Kukamilika kwa barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga Port na upanuzi wa bandari ya Kasanga ni mkakati wa Serikali wa kuhuisha uchumi katika mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi na hivyo kuchochea biashara kati ya Tanzania na nchi za Zambia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ( DRC).