TPA: NDEGE ZA KITALII ZITATUA BAHARINI

0
170

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Juma Kijavara amesema, mamlaka hiyo ina mpango wa kutekeleza mradi unaojulikana kama Dynamic Water Front katika bandari ya Dar es Salaam.

Mradi huo utakuwa na gati maalumu la utalii litakaloruhusu ndege kutua au kuanzia safari kwenye maji.

Akiwasilisha taarifa za kuanza kwa mradi huo kwa Naibu Waziri Uchukuzi David Kihenzile, Kijavara amesema moja ya maeneo muhimu katika mradi huo ni pamoja na eneo zitakapotua ndege za kitalii zinazoelekea Zanzibar, Mafia na maeneo mengine nchini.

Ameongesa kuwa pamoja na kuwa na gati maalumu la utalii, mradi huo pia utakuwa na eneo la hoteli kubwa za kisasa, maeneo ya kupumzika na eneo la kuhudumia meli kubwa.

Mradi huo wa Dynamic Water Front utagawanyika katika maeneo makubwa matano ambayo yote yatapatiwa majina ya wanyama wakubwa ambao ni tembo, chui, faru, simba na nyati.

Kijavara amesema mradi huo unaweza kuwa ni mkubwa pekee wenye huduma kama hizo kwa Afrika Mashariki na unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwishoni mwa mwaka huu.

Kwa sasa mradi huo upo katika hatua ya mazungumzo na mwekezaji ambaye watasirikiana kuutekeleza.