Timu yaundwa kufuatilia mikopo ya Wanafunzi

0
181

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeunda timu ya watu watatu, ambayo itakuwa ikifuatilia mwenendo katika utoaji wa mikopo kwa Wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

Taarifa ya kuundwa kwa timu hiyo imetolewa mkoani Dar es Salaam na waziri wa wizara hiyo Profesa Adolf Mkenda wakati wa mkutano wake na Wahariri wa vyombo vya habari.

Amesema tayari timu hiyo imeanza kazi na itafanya kazi hiyo kwa muda wa miaka mitano.

Amesema timu hiyo inaongozwa na Profesa Allan Mushi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe na atakuwa na Idd Makame kutoka Zanzibar pamoja na Dkt. Martin Chegele.

Profesa Mkenda ametaka mtu yeyote mwenye taarifa zozote iwe za malalamiko kuhusu mwenendo wa utoaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa Wanafunzi awasilishe taarifa hizo kwenye timu hiyo.