THBUB, LHRC wajipanga kutoa elimu mashuleni

0
390

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wamekubaliana kuandaa mpango wa pamoja wa kutoa elimu mashuleni, ili kuhamasisha na  kukuza haki za binadamu nchini.

Makubaliano hayo yamefikiwa jijini Dodoma na pande zote mbili baada ya majadiliano yaliyofanyika katika kikao kilichokutanisha ujumbe wa THBUB na viongozi wa LHRC.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma, Mafunzo, Utafiti na Nyaraka wa THBUB, Alexander Hassan amesema kuwa ili ushirikiano wa tume hiyo na LHRC uwe na tija ni vema kuunganisha nguvu katika maeneo wanayofanya kazi zinazofanana ili kupata matokeo makubwa zaidi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amesema kuwa suala hilo la kuunganisha nguvu ni zuri na ni muhimu likafanyiwa kazi haraka, na endapo uongozi wa THBUB utaridhia basi maafisa wa pande zote mbili wakutane ili kuandaa mpango huo.

Amesema kuwa kwa muda mrefu LHRC imekuwa ikitoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya haki za binadamu kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na matumizi ya vyombo vya habari, vipeperushi na mikutano ya hadhara na hivyo kuwafikia watu wengi, lakini ni muhimu kwa sasa kuunganisha nguvu na THBUB lengo likiwa ni kuepuka kutawanya nguvu na rasilimali kwa mambo ambayo wanaweza kufanya kwa pamoja.